Historia ya chuo

CHUO CHA UALIMU MONDULI

HISTORIA YA CHUO

Chuo cha Ualimu Monduli kilianzishwa mwaka 1971 kwa kubadili Shule ya Bweni iliyokuwa ‘ Monduli Middle School’ kuwa Chuo cha Ualimu. Nia na madhumuni ilikuwa kupata walimu wengi baada ya eneo hili la Masai kuanzisha Shule nyingi za msingi baada ya Uhuru.

Chuo kilianza katika hali rahisi na kubadilika kama ifuatavyo:

Mwaka 1971:

Chuo kilianza kwa kupokea wanachuo waliotokea Jeshi la kujenga Taifa(JKT) ambao walifunzwa ualimu kwa mwaka mmoja na kupewa cheo cha Mwalimu daraja D. Sifa ya kujiunga na mafunzo ya JKT ilikuwa darasa la VII. Uwezo wa Chuo ulikuwa wanachuo 120.

Mwaka 1975:

Kozi ya Ualimu Daraja D ilisitishwa na mafunzo kuwa ya miaka miwili na wahitimu walipewa cheti cha Mwalimu Daraja C. Sifa ya kujiunga ilikuwa darasa la saba bila masharti mengine. Uwezo wa Chuo ulikuwa wanachuo180.

Mwaka 1976 – 1978: 

Mradi wa kupanua Chuo ulitekelezwa kwa kujenga majengo mapya katika shamba la ng’ombe lililomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli. Mradi huo ulitekelezwa kwa msaada wa Serikali ya Denmark.

Mwaka 1979:

Chuo kilihamia majengo mapya. Wasichana walisajiliwa kwa mafunzo kwa mara ya kwanza. Kozi ya Ualimu Daraja IIIA ilianzishwa na kuendeshwa sambamba na ile ya Ualimu Daraja C. Uwezo wa Chuo ulikuwa wanachuo 600 kama ilivyo sasa.

Mwaka 1980: 

Kozi ya Diploma kwa somo la kilimo ilihamishiwa Chuo cha Ualimu Monduli kutoka Chuo cha Ualimu Butimba.

Mwaka 1983:

Mafunzo ya Elimu ya Sekondari kidato cha V na VI na Ualimu yalianzishwa ikiwa ni mbinu ya Serikali ya kupata walimu wa kutosha katika masomo ya Sayansi, Sayansi kilimo na Sayansi kimu. Muda wa mafunzo ulikuwa miaka mitatu. Idadi iliyoruhusiwa kwa kozi hii ilikuwa 160. Katika kipindi hiki, Chuo kilikuwa na mafunzo ya aina tatu (Daraja A kidato cha V & VI na Diploma ya Ualimu).

Mwaka 1992:

(a)  Mafunzo ya kidato cha V na VI yalifungwa na wanachuo wa Diploma   ya     Ualimu walitakiwa wachaguliwe kutoka Shule za Sekondari au Vyuo vya  Kilimo. Baada ya agizo hili kozi zote za Diploma zilikuwa za miaka miwili.

(b) Chuo cha Ualimu Monduli kilitakiwa kifundishe kozi zote za Sayansi zilizokuwa katika Chuo cha Ualimu Mkwawa (Iringa) ambacho kilifungwa na kurejeshwa tena kuwa shule ya Sekondari. Chuo cha Monduli kilipokea wanachuo 275 waliokuwa mwaka wa pili katika Chuo cha Ualimu Mkwawa. Uhamisho huu ulibadili mambo mengi hapa Monduli ikiwa ni pamoja na kupanuliwa kwa kozi za sayansi na kuongezwa wakufunzi.

Mwaka1997:

Wizara ya Elimu ilifunga kozi ya Ualimu Daraja A, na kuagiza Chuo cha Ualimu Monduli kiwe Chuo cha kozi za Sayansi tu kwa kiwango cha Diploma. Agizo hili lilifuatiliwa na uhamisho wa wakufunzi wote waliokuwa wakifundisha masomo  ya sanaa. Wengi wao walihamia Shule za Sekondari za jirani kuwa Wakuu wa  Shule. Masomo makuu yanayofundishwa katika kozi za Diploma hadi sasa ni Ualimu, Fizikia, Kemia, Biolojia, Hisabati, Jiografia, Kilimo, Sayansi kimu na ‘General studies’.

Mwaka 1998:

Wizara ya Elimu iliagiza Shule ya Sekondari Irkisongo iwe shule ya Mazoezi kwa ajili ya kozi za Diploma. Agizo hili lilipanua uwajibikaji katika eneo la taaluma na utawala kwani jamii ya Chuo ilipanuka kuwa na walimu wa Sekondari katika shule hiyo. Hivyo kuanzia kipindi hiki Chuo kimekuwa na shule mbili za mazoezi (msingi na Sekondari).

Mwaka 2000:  

Kozi ya Ualimu Daraja A ilirejeshwa kwa muda ili kutoa walimu wa   shule za msingi waliohitajika kwa wingi wakati wa programu ya kupanua   elimu ya msingi. Chuo kiliwezesha vijana wengi watokao mikoa ya Arusha na  Manyara kusomea ualimu karibu na kwao na wengi walipangwa kazi katika  mikoa hii ambayo inasemekana ina mazingira magumu. Mei 2005 mpango wa kufunza walimu wa Daraja A ulisitishwa.

Mwaka 2007 (Julai):

Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi ilitoa mtaala mpya kwa mafunzo ya    ualimu.Iliyokuwa inakazia taaluma na mbinu za ufundishaji. Changamoto kwa wizara ilikuwa kupata walimu wengi kwa shule za  Sekondari baada ya shule nyingi kuanzishwa katika kila kata nchi nzima. Pia kutoa walimu bora zaidi wanaomudu ufundishaji wa kisasa kwa kutumia teknolojia. Masomo mapya yalioongezwa katika mtaala huo ni:

  • Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kutumia Computer.
  • Stadi za Mawasiliano (Communication Skills).
  •  Teknolojia ya vielelezo (Media Technology).

Mwaka 2007/09:

Mabadiliko ya mitaala kwa stashahada ya ualimu wa sekondari yalifanyika. Mafunzo yalikuwa ya miaka miwili na yaliitwa ya stashahada ya ualimu wa sekondari. Wanachuo walikaa mwaka mmoja chuoni na walikwenda katika shule za sekondari kwa muda wa miezi minane kufundisha. Walirudi chuoni kufanya mitihani.

Mwaka 2008:

Chuo kilitoa tena mafunzo ya ualimu daraja IIIA. Wanachuo 217 walimaliza mafunzo yao Mei 2010.

Mwaka 2009/10 hadi sasa:

Wizara ilibadilisha tena muundo wa mafunzo na kuyafanya yawe ya miaka miwili chuoni.

Mafunzo mengine yaliyofanyika chuoni:

  1. Mafunzo ya kuwaendeleza walimu daraja III B/C kuwa IIIA (mwaka 2004- 2008)
  2. Mafunzo ya waelimisha walimu (maafisa elimu, wakufunzi, wakaguzi wa shule) mwaka 2003-2010.
  3. Mafunzo ya muda mfupi (induction programme) mwaka 2006/07.

Wahitimu wa Ualimu C.C.U Monduli

Mwaka Idadi ya wanafunzi
Diploma Cheti (IIIA) Cheti (IIIC)
1971 -1980       –      – 1079
1981 -1990   591 1889     85
1991 -2000 1524 1288      –
2001 -2010 2217   891      –
Mei 2011   369      –      –
Jumla 4701 4068 1164

WIMBO WA SHULE >> BOFYA HAPA